Full width home advertisement

Travel the world

Post Page Advertisement [Top]



Hotuba ya kwanza ya Mwalimu J.K. Nyerere alipokuwa Waziri mkuu baada ya Chama cha TANU kushinda uchaguzi na kuwa na jukumu la kuunda Baraza la kwanza la Mawaziri wa serikali ya Tanganyika mwaka 1961.

Wazee wangu
 Ndugu zangu,
Nadhani ni wajibu wangu kusema nanyi tena jioni hii ya kwanza baada ya kushika mzigo wa kuwa waziri mkuu wenu wa kwanza.

Labda mtafikiri kuwa kubadili jina tu, kutoka chief minister na kuitwa waziri mkuu si jambo la maana sana. Kwa kweli kubadili jina peke yake si jambo la maana sana.

Lakini natumaini kuwa wote mnaelewa ,maana jambo hili lilielezwa vizuri sana wakati wa mkutano wa machi kwamba ,kubadili jina  huku kunafuatana na mabadiliko katika utawala wa nchi yetu, ambayo Watanganyika wote tunastahili kujivunia.

Mabadiliko haya ya leo, yamekamilisha serikali yetu ya wananchi. Bwana Gavana ambaye ametusaidia sana alipokuwa mwenyekiti wa baraza la mawaziri ambao wote 11, nimewachagua mimi mwenyewe.

Nawaelezeni jambo hili kwa unyenyekevu mkubwa, kwa sasa mimi na wenzangu ni watumishi wenu nyinyi mnaonisikiliza. Tunajua kuwa mnatuamini, nanyi mnajua kuwa tunawaamini . na ni nyinyi tu mnaotupa nguvu zetu tunazozihitaji kwa kazi kubwa iliyoko mbele yetu.

Kwa msaada wa mwenyezi mungu na imani mliyo nayo juu yetu ,tunapata na tutazidi kupata nguvu za kuendesha serikali yenu. Lakini tunawaomba msisahau na mara nyingi sana nimekukumbusheni jambo hili kwamba serikali haiwezi kufanya kila kitu.

Utajiri wa Tanganyika bado uko ardhini. Hatuanzi na akiba kubwa ya fedha kama Ghana kwa mfano ,iliyoanza nayo ilipopata Uhuru wake. Hatuna mkononi fedha walizonazo ndugu zetu wa Nigeria.
Elimu yetu Iko nyuma zaidi kuliko Ghana, au Nigeria. Kwa kweli elimu yetu Iko nyuma zaidi kuliko Kenya na Uganda.

Kwa hiyo, tunaanza bila ya kuwa na wananchi wa kutosha wenye elimu ya  Juu tunayoihitaji katika jitihada zetu za kujenga utajiri wa nchi hii.
Lakini matatizo haya, hayanitishi mimi,hayawatishi wenzangu, na wala hatuombi kwamba, yawatisheni ninyi. Tunayaona kwamba ni jaribio tu. Lakini jaribio hili na umaskini Si la serikali tu, ni la kila raia wa Tanganyika.

Mara nyingi sana nimesema nanyi juu ya umaskini, ujinga na maradhi, lakini kwa kweli adui yetu mkubwa ni umaskini.
Tukiweza kumshinda adui huyu, tutakuwa tumeweza kupata silaha itakayotuwezesha kuushinda ujinga na maradhi.
Lakini ni ninyi tu, tunaoweza kupigana Vita ya umaskini. Namuomba kila raia wa Tanganyika, aape kiapo cha kuwa adui wa umaskini, Amshambulie adui huyo mahali popote atakapoonekana.

Ukiacha pamba yako shambani bila kuichuma, ukiwa na  uwezo wa kuongeza shamba lako kwa eka moja tu au nusu eka, au hata robo eka, lakini ukaacha kwa uvivu tu. Ukaacha rutuba ya shamba lako ikaharibiwa ,ikiwa shamba lako limejaa magugu na wewe hujishughulishi kuyaondoa, ukiwa unapuuza masharti unayopewa na wataalamu wa kilimo au hujishughulishi kuongeza elimu yako ya kilimo au  ikiwa unazurura tu bila kufanya kazi ,ukimtegemea Mjomba au shangazi, au waziri mkuu wa Tanganyika akufanyie kazi, basi wewe ndugu yangu si adui wa umaskini.

Wewe Si adui wa ujinga, wewe Si adui wa maradhi, wewe kwa kweli ni rafiki mkuu wa maadui hao.
Wewe ni adui wa watanganyika wote wanaofanya jitihada yao yote kumshambulia adui huyo.
Ndugu zangu ,vita hii ni yenu , vita hii ni yetu wote na adui yetu ni huyo niliyemtaja.
Basi tusipoteze wakati wetu tukipigana vita iliyokwisha. Tusipoteze wakati tukishambulia maadui ambao kwa sasa ni marehemu.

Tusidhani hata kidogo, sifa yetu katika afrika au sifa yetu katika dunia nzima ,itategemea ukali na ufundi wa matusi tutakayotumia kutukana ukoloni uliokufa au hata ukoloni mpya utakojaribu kuanzishwa kwa ujanja na hila za watu wasiopenda Uhuru wetu. Sifa yetu itategemea mambo tutakayofanya kuongeza na kudumisha nguvu zetu ili tuwe na uwezo wa kulinda Uhuru wetu wenyewe na pia kuwasaidia ndugu zetu wengine kupata Uhuru wao na kuulinda.

Wala tusipoteze wakati wetu katika kugombania vyeo na fahari ya nafsi. Kilichotufikisha hapa leo, kwa upesi hivi na kwa  amani hivi ni umoja wa watu wa Tanganyika. Ninapoulizwa kwa mfano, ni nini kilichotuwezesha kumaliza mkutano wa mwezi wa Machi kwa muda wa Siku mbili tu,  jibu langu ni moja , umoja.

Wenzangu na mimi tulikuwa kitu kimoja kwa sababu Tanganyika yenyewe ni kitu moja, Ni vilevile katika mambo yetu yote ya maisha ya taifa letu, Nani asiyejua kwamba msingi wa kufanikiwa kwa TANU, ni umoja wa TANU. Kadhalika katika vyama vya ushirika au vyama vya wafanyakazi wanachama wake wanaposhikana bega kwa bega mambo yao yatawaendea vyema.

Wanachama wake wakigombana na kutengana mambo yao na mambo ya taifa zima yatakwenda tenge.
Ndugu zangu huu si wakati wa kuchezea umoja wetu ,tunahitaji sasa kama tulivyouhitaji zamani kwa ajili ya kuinua hali zetu na ndugu zetu.

Lakini umoja hauhitajiwi na Tanganyika peke yake, afrika  nzima tunahitaji umoja. Kama mnavyojua nilikuwa Ghana na Nigeria, huko nilikutana na ndugu zangu na wote wanatutakia kheri na baraka .
Matembezi hayo yamenikumbusha tena uzito wa mzigo huu tulioanza kuubeba. Tutawezaje ndugu zangu kuubeba mzigo huu.
Tunaweza kuubeba kwa kuonyesha mfano tu, mfano wa taifa lenye umoja kamili ,lenye nia moja tu, kujenga taifa letu kwa manufaa ya watu wake wote.

Kusaidia ndugu zetu wa afrika popote walipo, kujenga udugu na mapenzi, baina yetu na binadamu wote .ikiwa ndugu zetu katika nchi za jirani wana tabu na tunajua wanazo taabu nyingi , wajibu wetu ni kutumia umoja wetu kuwasaidia wao pia.
Kila nilikokwenda nilipokuwa Ghana na Nigeria nilikumbushwa faida ya umoja. Ni wajibu wetu kuepukana na vishawishi vyote vya kuuvunja umoja wetu au kuleta utengano baina yetu na majirani zetu.

Najua kuwa,Uhuru huleta kishawishi cha kutengana na marafiki na majirani ili kuonyesha kwamba tuna nguvu sana, japo tukiwa peke yetu.
Hiki ni kishawishi cha kuepukwa kama ugonjwa ,kwa sababu tusipokiepuka tunaweza tukawadhuru ndugu zetu na tukiwadhuru wao nasi tutajidhuru.
Pana haja gani ndugu Zangu, kutumia Uhuru wetu kwa kutamba na kujitutumua mbele ya waafrika wenzetu. Hivyo ndivyo mataifa ya kizungu yalivyofanya na yakapata hasara kubwa sana.
Kabla ya utaifa kuanza, wazungu walikuwa na umoja mzuri sana, umoja huu uliharibiwa na kujitutumua kwa kila taifa kwa upande wake.

Leo ,ulaya haina umoja, wazungu wanajuta na wanafanya kila jitihada kuujenga tena umoja wao, ni umoja wajibu wetu ndugu zangu kujifunza kwa makosa yao, ni wajibu wetu kuchagua yaliyo mazuri na kuacha yaliyo mabaya.
Umoja ni jambo zuri ,basi na tuudumishe umoja wetu, lakini kujitenga na majirani ni jambo baya, basi na tuliepuke kosa hilo. Basi ndugu zangu, ndiyo mawazo niliyotaka kushirikiana nanyi jioni hii.

Kwanza ,kazi, kwani kazi peke yake itakayotuondolea umaskini wetu, pili , umoja , kwani bila umoja hatuna nguvu ya kuendelea na jambo lolote.
Tatu, udugu ,ili Uhuru usilete utengano baina yetu na waafrika wenzetu au binadamu wenzetu. Katika jitihada ya kutimiza shabaha hizo, mimi pamoja na wenzangu tutawatumikieni kwa uwezo wetu wote.
Na kwa msaada wa mwenyezi mungu ,tutajitahidi kuwatumikieni bila kujitafutia faida zetu wenyewe au fahari ya jambo Ndugu zangu, wazee wangu na akina mama, tupeni msaada wenu...

No comments:

Post a Comment

Bottom Ad [Post Page]